1Ndipo Mose na Waisraeli wakamwimbia Bwana wimbo huu:“Nitamwimbia Bwana,kwa kuwa ametukuzwa sana.Farasi na mpanda farasiamewatosa baharini.
2Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu;amekuwa wokovu wangu.Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu,Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza.
3Bwana ni shujaa wa vita;Bwana ndilo jina lake.
4Magari ya vita ya Farao na jeshi lakeamewatosa baharini.Maafisa wa Farao walio bora sanawamezamishwa katika Bahari ya Shamu.
5Maji yenye kina yamewafunika,wamezama mpaka vilindini kama jiwe.
6“Mkono wako wa kuume, Ee Bwanaulitukuka kwa uweza.Mkono wako wa kuume, Ee Bwana,ukamponda adui.
7Katika ukuu wa utukufu wako,ukawaangusha chini wale waliokupinga.Uliachia hasira yako kali,ikawateketeza kama kapi.
8Kwa pumzi ya pua zakomaji yalijilundika.Mawimbi ya maji yakasimama imara kama ukuta,vilindi vikagandamana ndani ya moyo wa bahari.
9“Adui alijivuna,‘Nitawafuatia, nitawapata.Nitagawanya nyara;nitajishibisha kwa wao.Nitafuta upanga wanguna mkono wangu utawaangamiza.’
10Lakini ulipuliza kwa pumzi yako,bahari ikawafunika.Wakazama kama risasikwenye maji makuu.
11“Ni nani miongoni mwa miungu aliye kama wewe, Ee Bwana?Ni nani kama Wewe:uliyetukuka katika utakatifu,
utishaye katika utukufu,
ukitenda maajabu?
12Uliunyoosha mkono wako wa kuumena nchi ikawameza.
13“Katika upendo wako usiokoma utawaongozawatu uliowakomboa.Katika nguvu zako utawaongozampaka makao yako matakatifu.
14Mataifa watasikia na kutetemeka,uchungu utawakamata watu wa Ufilisti.
15Wakuu wa Edomu wataogopa,viongozi wa Moabu watatetemeka kwa hofu,watu wa Kanaani watayeyuka,
16vitisho na hofu vitawaangukia.Kwa nguvu ya mkono wakowatatulia kama jiwe,mpaka watu wako waishe kupita, Ee Bwana,mpaka watu uliowanunua wapite.
17Utawaingiza na kuwapandikizajuu ya mlima wa urithi wako:hapo mahali, Ee Bwana, ulipopafanya kuwa makao yako,mahali patakatifu, Ee Bwana, ulipopajenga kwa mikono yako.
18Bwana atatawalamilele na milele.”
19Farasi wa Farao, magari yake ya vita na wapanda farasi wake walipoingia baharini, Bwana aliyarudisha maji ya bahari yakawafunika, lakini wana wa Israeli walipita baharini mahali pakavu.
20Kisha Miriamu yule nabii mke, ndugu yake Aroni, akachukua matari mkononi mwake na wanawake wote wakamfuata na matari yao wakicheza.
21Miriamu akawaimbia:“Mwimbieni Bwana,kwa maana ametukuka sana.Farasi na mpanda farasiamewatosa baharini.”
22Kisha Mose akawaongoza Israeli kutoka Bahari ya Shamu na kuingia katika Jangwa la Shuri. Kwa siku tatu walisafiri jangwani bila kupata maji.
23Walipofika Mara, hawakuweza kunywa maji yake kwa sababu yalikuwa machungu. (Ndiyo sababu mahali hapo panaitwa Mara*)
24Kwa hiyo watu wakamnungʼunikia Mose, wakisema, “Tunywe nini?”
25Ndipo Mose akamlilia Bwana, naye Bwana akamwonyesha kipande cha mti. Akakitupa ndani ya maji, nayo maji yakawa matamu. Huko Bwana akawapa amri na sheria na huko akawajaribu.
26Mungu akasema, “Kama mkisikiliza kwa bidii sauti ya Bwana Mungu wenu na kuyafanya yaliyo sawa machoni pake, kama mkiyatii maagizo yake na kuzishika amri zake zote, sitaleta juu yenu ugonjwa wowote niliowaletea Wamisri, kwa kuwa Mimi ndimi Bwana, niwaponyaye.”
27Kisha wakafika Elimu, mahali palipokuwa na chemchemi kumi na mbili, na miti sabini ya mitende, wakapiga kambi huko karibu na maji.
Tanbihi
Mara maana yake ni Chungu.