1Neno la Bwana likanijia kusema:
2“Mwanadamu, toa unabii na useme: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:“ ‘Ombolezeni ninyi na mseme,“Ole wa siku ile!”
3Kwa kuwa siku ile imekaribia,siku ya Bwana imekaribia,siku ya mawingu,siku ya maangamizi kwa mataifa.
4Upanga utakuja dhidi ya Misri,nayo maumivu makuu yataijia Ethiopia.Mauaji yatakapoangukia Misri,utajiri wake utachukuliwa
na misingi yake itabomolewa.
5Kushi*na Putu, Ludi na Arabia yote, Libya*na watu wa nchi ya Agano watauawa kwa upanga pamoja na Misri.
6“ ‘Hili ndilo Bwana asemalo:“ ‘Wale walioungana na Misri wataangukana kiburi cha nguvu zake kitashindwa.Kutoka Migdoli hadi Aswani,watauawa ndani yake kwa upanga,asema Bwana Mwenyezi.
7“ ‘Hizo nchi zitakua ukiwamiongoni mwa nchi zilizo ukiwa,nayo miji yao itakuwa magofumiongoni mwa miji iliyo magofu.
8Ndipo watakapojua kwamba mimi ndimi Bwana,nitakapoiwasha Misri moto
na wote wamsaidiao watapondwa.
9“ ‘Siku hiyo wajumbe watatoka kwangu kwa merikebu, ili kuwatia hofu Ethiopia, wakiwa katika hali yao ya kuridhika. Maumivu makali yatawapata siku ya maangamizi ya Misri, kwa kuwa hakika itakuja.
10“ ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:“ ‘Nitakomesha makundi ya wajeuri ya Misrikwa mkono wa Nebukadneza mfalme wa Babeli.
11Yeye na jeshi lake, taifa lililo katili kuliko mataifa yote,litaletwa ili kuangamiza nchi.Watafuta panga zao dhidi ya Misrina kuijaza nchi kwa waliouawa.
12Nitakausha vijito vya Nailina nitaiuza nchi kwa watu waovu,kwa mkono wa wageni,nitaifanya nchi ukiwa na kila kitu
kilichomo ndani yake.Mimi Bwana nimenena haya.
13“ ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:“ ‘Nitaangamiza sanamuna kukomesha vinyago katika Memfisi*Hapatakuwepo tena na mkuu katika nchi ya Misri,nami nitaeneza hofu katika nchi nzima.
14Nitaifanya Pathrosi*kuwa ukiwana kuitia moto Soani,
nami nitaipiga kwa adhabu Thebesi*
15Nitaimwaga ghadhabu yangu juu ya Pelusiumu,*ngome ya Misri,nami nitakatilia mbalimakundi ya wajeuri wa Thebesi.
16Nitaitia moto nchi ya Misri;Pelusiumu itagaagaa kwa maumivu makuu.Thebesi itachukuliwa na tufani,Memfisi itakuwa katika taabu daima.
17Wanaume vijana wa Oni*na wa Pi-Besethi*wataanguka kwa upanga
nayo hiyo miji itatekwa.
18Huko Tahpanhesi mchana utatiwa gizanitakapovunja kongwa la Misri;
hapo kiburi cha nguvu zake kitakoma.Atafunikwa na mawinguna vijiji vyake vitatekwa.
19Kwa hiyo nitaipiga Misri kwa adhabu,nao watajua kuwa Mimi ndimi Bwana.’ ”
20Katika mwaka wa kumi na moja, mwezi wa kwanza, siku ya saba, neno la Bwana likanijia kusema:
21“Mwanadamu, nimevunja mkono wa Farao mfalme wa Misri. Haukufungwa ili upone au kuwekewa kipande cha ubao ili upate nguvu za kuweza kuchukua upanga.
22Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Mimi ni kinyume na Farao mfalme wa Misri. Nitavunja mikono yake yote miwili, ule mkono ulio mzima pia na ule uliovunjika na kuufanya upanga uanguke toka mkononi mwake.
23Nitawatawanya Wamisri miongoni mwa mataifa na kuwafukuza huku na huko katika nchi zote.
24Nitaitia nguvu mikono ya mfalme wa Babeli na kuutia upanga wangu mkononi mwake, lakini nitavunja mikono ya Farao, naye atalia kwa huzuni mbele yake kama mtu aliyetiwa jeraha la kumfisha.
25Nitaitia nguvu mikono ya mfalme wa Babeli, lakini mikono ya Farao italegea. Ndipo watakapojua kwamba Mimi ndimi Bwana, nitakapoutia upanga wangu mkononi mwa mfalme wa Babeli, naye ataunyoosha dhidi ya Misri.
26Nitawatawanya Wamisri miongoni mwa mataifa na kuwafukuza huku na huko katika nchi mbalimbali. Ndipo watakapojua kwamba Mimi ndimi Bwana.”
Tanbihi
Kushi ndiyo Ethiopia.
Libya ndiyo Kubu.
Kiebrania ni Nofu.
Pathrosi ni Misri ya Juu.
Thebesi kwa Kiebrania ni No (au No-Amoni), mji katika Misri.
Kiebrania ni Sini.
Yaani Heliopoli (Mji wa Jua).
Yaani Bubasti.