1Mwimbieni Bwana wimbo mpya;mwimbieni Bwana dunia yote.
2Mwimbieni Bwana, lisifuni jina lake;tangazeni wokovu wake siku baada ya siku.
3Tangazeni utukufu wake katikati ya mataifa,matendo yake ya ajabu miongoni mwa mataifa yote.
4Kwa kuwa Bwana ni mkuu mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote;yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote.
5Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu,lakini Bwana aliziumba mbingu.
6Fahari na enzi viko mbele yake;nguvu na utukufu vimo patakatifu pake.
7Mpeni Bwana, enyi jamaa za mataifa,mpeni Bwana utukufu na nguvu.
8Mpeni Bwana utukufu unaostahili jina lake;leteni sadaka na mje katika nyua zake.
9Mwabuduni Bwana katika uzuri wa utakatifu wake;dunia yote na itetemeke mbele zake.
10Katikati ya mataifa semeni, “Bwana anatawala.”
Ulimwengu ameuweka imara, hauwezi kusogezwa;atawahukumu watu kwa uadilifu.
11Mbingu na zishangilie, nchi na ifurahi;bahari na ivume, na vyote vilivyomo ndani yake;
12mashamba na yashangilie,pamoja na vyote vilivyomo ndani yake.Kisha miti yote ya msituni itaimba kwa furaha;
13itaimba mbele za Bwana kwa maana anakuja,
anakuja kuihukumu dunia.Ataihukumu dunia kwa haki,na mataifa katika kweli yake.