1Misemo ya Mfalme Lemueli, usia wa mama yake aliyomfundisha:
2“Ee mwanangu, ee mwana wa tumbo langu,ee mwana wa nadhiri zangu,*
3Usitumie nguvu zako kwa wanawake,uhodari wako kwa wale wanaowaharibu wafalme.
4“Ee Lemueli, haifai wafalme,haifai wafalme kunywa mvinyo,
haifai watawala kutamani sana kileo,
5wasije wakanywa na kusahau vile sheria inavyoamuruna kuwanyima haki zao wote walioonewa.
6Wape kileo wale wanaoangamia,mvinyo wale walio na uchungu,
7Wanywe na kusahau umaskini waona wasikumbuke taabu yao tena.
8“Sema kwa ajili ya wale wasioweza kujisemea,kwa ajili ya haki za wote walioachwa ukiwa.
9Sema na uamue kwa haki,tetea haki za maskini na wahitaji.”
10Mke mwenye sifa nzuri, ni nani awezaye kumpata?Yeye ni wa thamani sana kuliko marijani.*
11Mume wake anamwamini kikamilifuwala hakosi kitu chochote cha thamani.
12Humtendea mumewe mema, wala si mabaya,siku zote za maisha yake.
13Huchagua sufu na kitaninaye hufanya kazi kwa mikono yenye bidii.
14Yeye ni kama meli za biasharaakileta chakula chake kutoka mbali.
15Yeye huamka kungali bado gizahuwapa jamaa yake chakula
na mafungu kwa watumishi wake wa kike.
16Huangalia shamba na kulinunua,kutokana na mapato yake hupanda shamba la mizabibu.
17Hufanya kazi zake kwa nguvu,mikono yake ina nguvu kwa ajili ya kazi zake.
18Huona kwamba biashara yake ina faida,wala taa yake haizimiki usiku.
19Huweka mikono yake kwenye pia,navyo vidole vyake hushikilia kijiti chenye uzi.
20Huwanyooshea maskini mikono yakena kuwakunjulia wahitaji vitanga vyake.
21Theluji ishukapo, hana hofu kwa ajili ya watu wa nyumbani mwake,kwa maana wote wamevikwa nguo za kutia joto.
22Hutengeneza mazulia ya urembo ya kufunika kitanda chake,yeye huvaa kitani safi na urujuani.
23Mume wake anaheshimiwa kwenye lango la mji,aketipo miongoni mwa wazee wa nchi.
24Hutengeneza mavazi ya kitani na kuyauza,naye huwauzia wafanyabiashara mishipi.
25Amevikwa nguvu na heshima,anaweza kucheka bila kuwa na hofu kwa siku zijazo.
26Huzungumza kwa hekimana mafundisho ya kuaminika yapo ulimini mwake.
27Huangalia mambo ya nyumbani mwakewala hali chakula cha uvivu.
28Watoto wake huamka na kumwita aliyebarikiwa,mumewe pia humsifu, akisema:
29“Wanawake wengi hufanya vitu vyenye sifa nzuri,lakini wewe umewapita wote.”
30Kujipamba ili kuvutia ni udanganyifu na uzuri unapita upesi,bali mwanamke anayemcha Bwana atasifiwa.
31Mpe thawabu anayostahili,nazo kazi zake na zimletee sifa kwenye lango la mji.
Tanbihi
Au: Ewe uliye jibu la maombi yangu.
Mithali 31:10-31 imetungwa kila mstari ukianzia na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.