Inapakia...
📖

Biblia Takatifu

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™
BIB 18 mistari

Zaburi 115

Zaburi • Sura 115 / 150

Mungu Mmoja Wa Kweli

1Sio kwetu sisi, Ee Bwana, sio kwetu sisi,bali utukufu ni kwa jina lako,kwa sababu ya upendona uaminifu wako.

2Kwa nini mataifa waseme,“Yuko wapi Mungu wao?”

3Mungu wetu yuko mbinguni,naye hufanya lolote limpendezalo.

4Lakini sanamu zao ni za fedha na dhahabu,zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu.

5Zina vinywa, lakini haziwezi kusema,zina macho, lakini haziwezi kuona;

6zina masikio, lakini haziwezi kusikia,zina pua, lakini haziwezi kunusa;

7zina mikono, lakini haziwezi kupapasa,zina miguu, lakini haziwezi kutembea;
wala koo zao haziwezi kutoa sauti.

8Wale wanaozitengeneza watafanana nazo,vivyo hivyo wale wote wanaozitumainia.

9Ee nyumba ya Israeli, mtumainini Bwana,yeye ni msaada na ngao yao.

10Ee nyumba ya Aroni, mtumainini Bwana,yeye ni msaada na ngao yao.

11Ninyi mnaomcha, mtumainini Bwana,yeye ni msaada na ngao yao.

12Bwana anatukumbuka na atatubariki:ataibariki nyumba ya Israeli,
ataibariki nyumba ya Aroni,

13atawabariki wale wanaomcha Bwana,wadogo kwa wakubwa.

14Bwana na awawezeshe kuongezeka,ninyi na watoto wenu.

15Mbarikiwe na BwanaMuumba wa mbingu na dunia.

16Mbingu zilizo juu sana ni mali ya Bwana,lakini dunia amempa mwanadamu.

17Sio wafu wanaomsifu Bwana,wale washukao mahali pa kimya,*

18bali ni sisi tunaomtukuza Bwana,sasa na hata milele.
Msifuni Bwana.*

Tanbihi

*

Mahali pa kimya maana yake ni Kuzimu, yaani Sheol kwa Kiebrania.

*

Msifuni Bwana ni Kiebrania Hallelu Yah.