Inapakia...
📖

Biblia Takatifu

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™
BIB 16 mistari

Zaburi 91

Zaburi • Sura 91 / 150

Mungu Mlinzi Wetu

1Yeye akaaye mahali pa salama pake Yeye Aliye Juu Sana,atadumu katika uvuli wake Mwenyezi.*

2Nitasema kumhusu Bwana, “Yeye ndiye kimbilio langu na ngome yangu,Mungu wangu, ambaye ninamtumaini.”

3Hakika yeye ataniokoa na mtego wa mwindaji,na maradhi ya kuambukiza ya kuua.

4Atakufunika kwa manyoya yake,chini ya mbawa zake utapata kimbilio,
uaminifu wake utakuwa ngao na kinga yako.

5Hutaogopa vitisho vya usiku,wala mshale urukao mchana,

6wala maradhi ya kuambukizayanayonyemelea gizani,
wala tauni iharibuyo adhuhuri.

7Ijapo watu elfu wataangukia kando yako,kumi elfu mkono wako wa kuume,
lakini haitakukaribia wewe.

8Utatazama tu kwa macho yakona kuona adhabu ya waovu.

9Kama ukimfanya Aliye Juu Sana kuwa makao yako:naam, Bwana ambaye ni kimbilio langu,

10basi hakuna madhara yatakayokupata wewe,hakuna maafa yataikaribia hema yako.

11Kwa kuwa atawaagiza malaika zake kwa ajili yako,wakulinde katika njia zako zote.

12Mikononi mwao watakuinua,ili usijikwae mguu wako kwenye jiwe.

13Utawakanyaga simba na nyoka wakali,simba mkubwa na nyoka utawaponda kwa miguu.

14Bwana asema, “Kwa kuwa ananipenda, nitamwokoa;nitamlinda, kwa kuwa analikiri Jina langu.

15Ataniita, nami nitamjibu;nitakuwa pamoja naye katika taabu,
nitamwokoa na kumheshimu.

16Kwa siku nyingi nitamshibishana kumwonyesha wokovu wangu.”

Tanbihi

*

Mwenyezi hapa ina maana ya Shaddai kwa Kiebrania.